JAMES WA FACEBOOK 21 - 25


 


JAMES WA FACEBOOK πŸ’‘ 21


“Ooooh Mungu ahsante sana” alisema Ramla huku akinyanyua mikono yote juu, angalau alitabasamu baada ya kujua Majeruhi yupo sawa.

“Kwahiyo kinachoendelea ni nini?” 

“Ulipaswa kupata PF3 Kutoka Polisi lakini kwakua imetokea muda mrefu atatibiwa tu hakuna shida, cha Msingi ni ukaribu wako kwetu sisi, usimtelekeza Majeruhi Tafadhali” alisistiza Daktari, Ramla akatabasamu


“Dokta, Mimi si Mtu wa hivyo. Kama wewe usingelitoka basi ningelikaa hapa hata siku tatu. Moyo wangu hauna hata chembe ya Ukatili” Walizungumza mengi, Suzy na Ramla walirudi nyumbani baada ya kulipa bili ya siku nzima ya pale Hospitalini, pesa haikua tatizo kwake.


Majira ya saa sita usiku, James alirejesha fahamu zake. Kwa dakika zaidi ya mbili alijishangaa alikua wapi, mwili ulijaa maumivu kila kiungo.


°°°′°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°


 JAMES WA FACEBOOK πŸ’‘ 22


Baadaye alikumbuka kikichomfika, chozi likambubujika. Hakujua ni Nani aliyemleta hapo Hospitalini, mara aliingia Daktari, kitu cha kwanza alichomweleza Daktari kilikua ni njaa kali iliyomsokota kwa zaidi ya siku nzima


Daktari akamkalisha vizuri James, kisha akampatia Uji wenye virutubisho ili apate nguvu, baada ya kufakamia uji Daktari alikaa na James na kuanza kumhoji

“Unaitwa Nani?” James alifikiria sana kumjibu Daktari, hofu yake kubwa ikawa ni pengine ataambiwa alipe bili za Hospitali, basi James akataja jina la Uwongo 

“Betrody” akataja jina la rafiki yake aliyemwacha Kijijini, akilini mwake James alijua akitaja jina halisi itamletea shida pale atakapotaka kutoroka hapo Hospitalini ili akwepe kulipa Bili.


“Pole sana Betrody, najua unakumbuka kua ulipata ajali mbaya ya kugongwa na gari, aliyekusababishia ametoka hapa na giza hili, amesema atakuja kesho” alisema Daktari, moyoni James akajilaumu kwanini alitaja jina tofauti wakati yupo wa kulipa Bili za Hospitalini.


°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°


JAMES WA FACEBOOK πŸ’‘ 23


“Sawa”

“Usijali utakua sawa, je ndugu zako tunawapataje?” swali hili lilimkumbusha kauli ya Mama yake, hakutaka kurudi tena Kijijini kwao kwa hofu mbili, kwanza kuchekwa na Betrody pili lawama kutoka kwa Mama yake sababu alitoroka, akilini James akawa na wazo atakapokutana na aliyemsababishia ajali hiyo amwombe amtafutie kazi.

“Sina ndugu hapa Mjini, ndugu zangu wapo Mkoani” 


“Sawa ugua pole, upumzike” alisema Daktari kisha aliondoka. Upande mmoja James alifurahi kupata ile ajali sababu inaweza kua fursa ya kuanza maisha mapya kupitia kwa aliyemsababishia Ajali, alilala akiwa ana tabasamu.


Asubuhi Mapema sana, Ramla alifika Hospitalini, sifa kubwa ya Ramla ilikua ni kuvaa nguo za stara za gharama kubwa sana, alipendelea mawani nyeusi anapokua anatoka nyumbani kwake, moja kwa moja alionana kwanza na Daktari ambaye alimpa ruhusa ya kwenda wodini kumwona Majeruhi wake.


Akiwa amevalia kiatu kirefu alipiga hatua za haraka hadi wodini, alipoyatupa macho yake kitandani alimwona James  akiwa anamtazama, Ramla akatabasamu hadi alipo James. Kitu cha kwanza aligundua Majeruhi alikua ni Mdogo kiumri kwake

“Hujambo?”


°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°


JAMES WA FACEBOOK πŸ’‘ 24


“Sijambo Shikamoo” 

“Marahaba, pole kwa maumivu Mdogo wangu” alisema Ramla

“Ahsante, wewe ndiye uliye nigonga na gari?”

“Ndiyo lakini ni Bahati mbaya tu sikukusudia”  


“Hamna shida najisikia nafuu, maumivu ya kichwa kwa mbali tu” alisema James akiwa anatabasamu

“Unaitwa Nani?” James akawaza kusema jina halisi lakini akaona ni bora ataje jina alilomwambia Daktari ili kukwepesha mgongano

“Naitwa Betrody”

“Oooh Naitwa Dada Ramla, hivi unaishi wapi Betrody?”


Swali hili lilikua linafanana na lile la Daktari, hakutaka kuipoteza nafasi, James akajibu huku akitia huruma

“Sina mahali pa kuishi, naranda randa mtaani tu, linapokucha jua ndipo ninapolala” alisema James

“Mungu wangu ni kweli?”

“Ndiyo ni kweli, sina mahali pa kuishi, nimekuja kutafuta Maisha hapa Mjini” alizidi kutia huruma James, Ramla alimfikiria sana James aliyejitambulisha kwake kama Betrody


“Basi usijali Betrody, pona kwanza nitajua cha kufanya” alisema Ramla kisha aliondoka Hospitalini huku akiumiza kichwa atamsaidia vipi Majeruhi wake, aliporudi nyumbani alimweleza Suzy


°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°°


 JAMES WA FACEBOOK πŸ’‘ 25


“Ulisema nisimwamini Mtu wa Mtandaoni, leo unamwamini Mtu uliyekutana naye barabarani” akasema Suzy huku akitabasamu

“Sasa nitafanya nini Suzy, unaujua moyo wangu ilivyo na huruma, kwakua Mume wangu hayupo na atakaa nje kwa miezi mingi nafikiria kumchukua aishi hapa nyumbani huku naangalia nimtafutie kazi, baada ya muda awe na Maisha yake ili niutuwe mzigo” alieleza Ramla huku akijishika kiuno chake.


“Siyo wazo baya Mwaya, mie hapa nina maumivu na yule Mjinga aliyekula pesa yangu akatokomea zake na hapatikani kwenye simu” walicheka kwa pamoja wakiwa wanazidi kuchakata stori za hapa na pale

Baada ya siku nne, aliruhusiwa kumchukua James Hospitalini mara baada ya Daktari kuthibitisha kuimarika kwa afya ya James.


 Alienda naye hadi nyumbani kwake, akawaambia Mlinzi na Msichana wa kazi juu ya mkasa uliotokea, japo alishamweleza Mume wake kila kitu lakini hakumweleza kua atamchukua James.


Moyo wa James kuna namna ulishusha pumzi, ile ajali ikawa mkombozi kwake, akaingia kwenye nyumba nzuri yenye hadhi, vyakula vingi vya kuchagua, hewa nzuri, chumba kizuri cha kulala, alitabasamu akiwa anaanza Maisha mapya.


Comments